Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa Watanzania kulinda utamaduni na utu wao na daima wasiudhalilishe dhidi ya utamaduni wa kigeni.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Februari 29,2024 wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mfuko huo.
“Kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi, kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni wetu ambao ni mzuri.” Amesema Dkt. Biteko
Aidha Dkt. Biteko amewasifu wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi zao za sanaa.
Amesema kuwa, wasanii wanao wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai, kuliondoa kwenye wimbi la kupotea duniani na kuwafanya watanzania waone lugha yao, tamaduni zao na desturi za Tanzania zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.
Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kazi ya Sanaa ilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza ajira na ndio maana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kuufufua mfuko huo ambao ulianzishwa tangu mwaka 1992 na ulikuwa ukisuasua lakini sasa umeimarika.
Dkt.Biteko amepongeza wasanii wote ambao wamekuwa wakizingatia vigezo na mashati ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuwataka wasanii kuhimizana juu ya umuhimu wa kukopa na kurejesha mikopo ili iweze kuwanufaisha wengine.
Amesema pamoja na ukweli kwamba Sekta ya Utamaduni na Sanaa inaongoza kwa ukuaji kati ya sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 lakini bado mchango wake kwa pato la Taifa ni duni kwani inachangia asilimia 0.3 na hii ikimaanisha kuwa Sekta inakua lakini haichangii zaidi.
Aidha ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuweka mazingira mazuri kwa wasanii ili kukuza sekta ya Utamaduni na Sanaa sambamba na ukuaji wa uchumi.