Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchema, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu.
Dkt. Nchemba alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo ngazi ya Juu.
Alisema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu imedhamiria kuwa na maendeleo endelevu ambayo hayamuachi Mtanzania yoyote nyuma kwa kufanya uwekezaji katika Sekta za Uzalishaji.
“Kipaumbele kimewekwa kwenye uwekezaji katika mtaji wa binadamu, maendeleo ya miundombinu, kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, utawala bora, kuwawezesha wanawake na uhifadhi wa mazingira”, alibainisha Mhe. Nchemba.
Alisema kuwa kwa kutekeleza mikakati hiyo pamoja na kukuza ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kuelekea kufikia ukuaji wa Uchumi endelevu.
Dkt. Nchemba alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ukuaji wa biashara, kuongeza ushindani na kukuza ubunifu ili kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, Dkt. Nchemba, alisema Tanzania pia inatumia Diplomasia ya Kiuchumi kama mkakati muhimu wa kuendeleza uchumi wake na kubainisha kuwa nchi ina dhamira kubwa ya kufuata kanuni za ushirikiano wa kimataifa wenye manufaa kwa pande zote.
Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. David Concar, alisema kuwa wadau wa maendeleo wanampongeza Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoyafanya na wanayaona mabadiliko mbalimbali anayofanya katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, biashara pamoja na uwekezaji katika sekta ya uzalishaji.
Alisema kuwa wadau wa maendeleo wako tayari kuendelea kuiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kukuza uchumi wa wananchi.