Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanywa na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo walisema licha ya kupata huduma za matibabu pia wamefurahia kupata elimu ya lishe ambayo imewasaidia kufahamu namna bora ya kuchagua makundi ya vyakula.
Mzee Abdalah Yasini mkazi wa Temeke alisema inawezekana kupatwa kwake kwa tatizo la mishipa ya damu kuziba kulisababishwa na kutokupata elimu ya lishe bora kwani angejua toka zamani namna ya kula chakula chenye mchanganyiko wa makundi yote ya vyakula kwa kiasi angeweza kuepuka tatizo la mishipa yake ya damu kuziba.
“Ninawaomba wataalamu wa lishe watafute namna ya kufikisha elimu ya lishe bora kwa jamii hata ikiwezekana katika vyombo vya habari kuwe na kipindi cha lishe kitatusaidia sana”, alisema Mzee Abdalah
“Elimu niliyoipata leo itaenda kunisaidia kwani nilikuwa najitahidi kupambana kupunguza uzito kwa kutumia njia ambayo si sahihi, nilikuwa sili milo ya asubuhi na mchana nakula usiku tu lakini nilivyofika hapa mtaalamu amenipa maelekezo kuwa ninapokula jioni na kwenda kulala sehemu kubwa ya chakula hutunzwa kama mafuta”, alisema Yusta
Yusta alisema mtaalamu wa lishe amemshauri kupunguza mlo wa jioni na namna ya kupata chakula bora kuanzi mlo wa asubuhi hadi jioni huku akimpa mbinu za kupunguza uzito wake bila ya kuleta athari nyingine za kiafya.
“Kwakweli elimu niliyoipata leo haitakuwa ya msaada kwangu tu bali ninaenda kuisaidia familia yangu kwasababu mimi ndio mama yao na mimi ndio mpishi hivyo ninaenda kuwasaidi pia katika kuboresha afya zao”, alisema Yusta
Mkuu wa Kitengo cha Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Maria Samlongo alisema wamekuwa wakitoa elimu ya lishe bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo pamoja na wananchi wanaohudumiwa katika kambi ambazo wamekuwa wakizifanya.