Wanawake wawili wenye umri wa miaka 60 na 65, wanaotuhumiwa uchawi, wamepigwa mawe na kisha kuchomwa moto hadharani siku ya Jumapili katika kijiji cha Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na vyanzo kadhaa vilivyohojiwa siku ya Jumatatu.
Wakati wa usiku, kundi la vijana kutoka Nyamutiri “waliwapiga mawe wanawake hawa na kuchoma miili yao baada ya kuwatoa nje ya nyumba zao”, kulingana na shirika la habari la AFP, likimnuku André Byadunia, kiongozi wa shirika la kiraia huko Uvira, makao makuu ya eneo ambapo matukio yalifanyika. .
Alibainisha kuwa wanawake hawa wawili waliuawa kwa sababu walituhumiwa na sehemu ya watu kufanya uchawi na “kuhusika na vifo vya watu kadhaa” katika jamii.
“Jivu linaondolewa kwenye eneo la mkasa,” amesema Makelele Murande, katibu tawala wa kichifu cha Bafuliru, ambapo wanawake hao wawili waliuawa, amehojiwa kwa njia ya simu Jumatatu mchana. “Polisi na jeshi hawakuweza kuingilia kati kwa wakati ili kuwaokoa wanawake hawa wawili,” amelaumu naibu mkuu wa eneo la Uvira, Timothée Bakanirwa.
Maandamano yalizuka baadaye, yaliyoandaliwa na “watu waliowaua” wanawake hao wawili, ameeleza Kelvin Bwija, kiongozi wa mashirika ya kiraia katika eneo hilo. Kulingana mwanaharakati huyo, waandamanaji walilalamika kwamba “wachawi wanaodaiwa kukamatwa kila mara huachiliwa na idara za usalama.”