Kiongozi wa kundi la uhalifu nchini Haiti Jim Cherizier anayedaiwa kuhusika na jaribio la kumpindua Ariel Henry Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametahadharisha juu ya uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa kwenye iwapo Henry hatajiuzulu.
Wahalifu wenye silaha ambao sasa wanadhibiti maeneo mengi ya Haiti walipanga jaribio la pamoja la kumuondoa mamlakani Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati alipokuwa nje ya nchi wiki iliyopita.
Ariel Henry Waziri Mkuu wa Haiti ambaye alipasa kuondoka madarakani mwezi Februari mwaka huu jana aripotiwa kuwa ameonekana huko Puerto Rico baada ya Jamhuri ya Dominican kukataa kutoa kibali kwa ndege yake ili kutua nchini humo.
Kiongozi huyo wa kundi la uhalifu nchini Haiti amesema kuwa iwapo Waziri Mkuu wa nchi hiyo hatajiuzulu na jamii ya kimataifa kuendelea kumuunga mkono basi nchi hiyo itakuwa inaelekea moja kwa moja katika vita vya ndani vitakavyosababisha mauaji ya kimbari.
Cherizier aliye na umri wa miaka 46 ambaye ni afisa wa zamani wa polisi anakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa kukiuka haki za binadamu huko Haiti.