Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani ghasia wanazosema zilitolewa na wanajeshi wa Israel wiki iliyopita dhidi ya Wapalestina waliokusanyika katika mji wa Gaza kukusanya unga kama “mauaji”.
Katika taarifa yake, kundi la wanahabari maalum wa Umoja wa Mataifa limeishutumu Israel kwa “kuwaua njaa kwa makusudi watu wa Palestina huko Gaza tangu Oktoba 8,” na kuongeza: “Sasa inawalenga raia wanaotafuta misaada ya kibinadamu na misafara ya kibinadamu.”
“Israel lazima ikomeshe kampeni yake ya njaa na kulenga raia,” walisema wataalamu wa Umoja wa Mataifa, ambao walionya kuna ushahidi unaoongezeka wa njaa katika Ukanda wa Gaza.
Takriban watu 112 walikufa na 760 walijeruhiwa siku ya Alhamisi wakati umati wa watu waliokata tamaa ulikusanyika kukusanya unga.
Mashahidi huko Gaza na baadhi ya waliojeruhiwa walisema kuwa vikosi vya Israel vilifyatua risasi kwa umati na kusababisha hofu. Israel ilisema watu walikufa kwa mshituko au wakanyagwa na lori za misaada ingawa ilikiri kuwa wanajeshi wake walifyatua risasi kwa kile ilichokiita “makundi”.
“Shambulio hilo limekuja baada ya Israel kukataa msaada wa kibinadamu katika mji wa Gaza na kaskazini mwa Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja,” walisema wataalam hao, ambao walielezea “mtindo wa mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Palestina wanaotafuta msaada”.