Vita nchini Sudan vinatishia kuzusha “janga kubwa zaidi la njaa duniani”, shirika la Umoja wa Mataifa limeonya.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema Jumatano kwamba zaidi ya watu milioni 25 waliotawanyika kote Sudan, Sudan Kusini na Chad “wamenaswa katika msururu” wa uhaba wa chakula.
Hata hivyo, vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe havionyeshi dalili ya kulegeza kamba baada ya miezi 10 ya mapigano.
“Vurugu zisizoisha” zinawafanya wafanyakazi wa misaada kushindwa kufikia asilimia 90 ya watu wanaokabiliwa na “viwango vya dharura vya njaa,” WFP iliongeza.
Akihitimisha ziara yake nchini Sudan Kusini, mkurugenzi mtendaji wa WFP Cindy McCain alisema: “Mamilioni ya maisha na amani na utulivu wa eneo zima ziko hatarini.”