Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi wa nchi za Afrika wamekubaliana kuhakikisha wanakusanya na kutumia rasilimali zilizopo vizuri pamoja na kuboresha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa Mjini Victoria Falls, Zimbabwe na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi kutoka Afrika unaoratibiwa na Kamisheni ya Uchumi wa Afrika chini ya Umoja wa Mataifa (UNECA)
Bw. Mwandumbya alisema kuwa kupatikana kwa rasilimali za kutosha kutawezesha Serikali kuhudumia miradi, kutimiza malengo ya kibajeti pamoja na kulipa madeni ya Serikali.
“Tumekuwa na sauti ya pamoja ya kuhakikisha tunaboresha Sheria, kanuni na usimamizi wa taasisi zetu za kukusanya mapato ili kuhakikisha tunaongeza mapato zaidi kutoka kwenye vyanzo vyetu, kwa kuwa upatikanaji wa rasilimali kutoka nje kwa njia ya mikopo na misaada imekuwa na changamoto kubwa,”alisema Mwandumbya
Bw. Mwandumbya alifafanua kuwa katika mkutano huo imewekwa mikakati mbalimbali itakayosaidia kujenga uwezo kwenye taasisi zilizopo ndani ya nchi za Afrika ili kuwa na uwezo thabiti wa kufanikisha malengo ya nchi husika.