Waathiriwa mbalimbali wamekuwa wakidai kwa zaidi ya miaka 20 kuundwa kwa mahakama maalum ya kuwahukumu wahusika wa uhalifu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 250,000.
Bunge la Libeŕia lilipitisha hoja juu ya hili, na kuongeza matumaini ya Walibeŕia kuwa hatimaye kuweza kushuhudia haki katika ardhi yao.
Hadi sasa, mahakama za kigeni zina jukumu la kuwashtaki wababe wa zamani wa vita. Paris kwa sasa inamhukumu kamanda wa zamani wa waasi Kunti Kamara katika ngazi ya rufaa.
Sasa jukumu hilo linaweza kuangukia Liberia yenyewe, kutokana na hoja iliyopitishwa siku ya Jumanne, ambayo inaleta matumaini na mashaka.
Mwanaharakati wa haki za binadamu Maxson Kpakio amekuwa akisubiri kuundwa kwa mamlaka hiyo tangu mwaka 2009. Mwaka huo, Tume ya Ukweli na Maridhiano ilichapisha ripoti iliyopendekeza kufunguliwa mashtaka kwa wahalifu dhidi ya ubinadamu. Pendekezo halikufanyiwa kazi.
Kwa hoja iliyopitishwa na Bunge la Liberia, matumaini ya haki yanazaliwa upya kwa Maxson Kpakio, ambaye alimpoteza mjomba wake wakati wa vita vya kwanza vya wenyewe kwa wenyewe, katika eneo la Lofa, mojawapo ya mikoa kulikoripotiwa mauaji mengi.
“Moja wapo ya makundi yanayopigana yalijaribu kumsajili mjomba wangu, lakini alikataa. Alisema dini yake haikumruhusu kuua, anasema Maxson Kpakio.
Walimfunga, wakamfunika macho na kumtesa,walimtia katika maji yanayochemka na ndivyo alivyouawa, kwa sababu tu alikataa kushiriki katika vita. “