Katika kuelekea kilele cha Wiki ya Wanawake Duniani Mamlaka ya Bandari ya TPA kupitia makao makuu ya Dar es Salaam, Watumishi Wanawake wametoa misaada mbalimbali yenye thamani ya Shilingi Milioni 60 katika kituo cha kulea Watoto yatima Jeshi la Wokovu, Kurasini na Hospitali ya Ocean Road.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam Mrisho Mrisho amewataka Wanawake kuzidisha upendo wa kutoa kwa wenye uhitaji kwani hiyo ni njia mojawapo ya kumsaidia Mhe. Rais Samia katika Sekta tofauti tofauti hasa katika Sekta ya Afya kama ambavyo mmefanya.
” Kwanza nawapongeza waliokuja na wazo hili lakini sisi kama Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam kupitia kwa Watumishi Wanawake tumeona tutoe tulichobarikiwa lakini hii si Mwisho huu mwanzo wetu kuna mengi tutafanya katika kumsaidia Mhe Rais kuijenga nchi” Amesema Mrisho
Naye Meneja Rasilimali watu Bandari ya Dar es Salaam Mwajuma Mkonga amesema katika Maadhimisho hayo wameona waanze kwa kushiriki matendo ya huruma katika Taasisi hizo, Wanawake hao walishiriki katika zoezi la uchunguzi wa Saratani ya matiti na mlango wa kizazi katika Kituo cha Afya cha TPA linaloratibiwa na Kituo hicho pamoja na Chama cha Madaktari wanawake Tanzania ( MEWATA)
Hata hivyo Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi kutoka Hospitali ya Ocean Road Marry Haule, amewatoa hofu kuwa Vifaa Tiba vyote vitaenda kutumika kama ambavyo wamepokea maelekezo kutoka kwao sambamba na kuwashukuru Watumishi Wanawake wa Mamlaka ya Bandari TPA kwa namna ambavyo wamekuwa na moyo wa huruma katika kusaidia jamii hasa kwa wale wenye uhitaji zaidi.
Msaada ambayo umetolewa na Mamlaka ya Bandari TPA ni mjumuisho wa Mahitaji mbalimbali kwa watoto yatima na vifaa tiba kwa matumizi ya Hospitali huku Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa Mwaka huu 2024 ikisema “ Wekeza kwa Wanawake Kurahisisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”.