Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani mashambulizi yanayozidi kuripotiwa kaskazini mwa Nigeria ambapo watoto wadogo na kina mama wamelengwa na wapiganaji wa kundi la Boko Haramu kwa kutekwa nyara.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Moussa Faki Mahamati amewataka ,‘”waliotekeleza uhalifu huo kuwarejesha watoto waliotekwa mara moja kwa familia zao”.
Ameendelea kusema kwamba, kitendo hicho ni ishara kwamba tishio la ugaidi na wizi wa mifugo ni masuala yanayotishia sio tu usalama wa eneo la kaskazini mwa Nigeria, bali eneo zima na hata mataifa jirani na ni jambo ambalo linasikitisha wote barani Afrika.’
Haya yanajiri wakati ambapo wanafunzi 15 walitekwa nyara Jumamosi, katika eneo la Gada, katika jimbo la Sokoto, kaskazini mwa Nigeria.
Mbunge wa eneo amesema kuwa,shambulizi hilo lilitokea alfajiri, ambapo wapiganaji pia waliwateka wanawake wanne.