Chama tawala cha Rwanda, Rwanda Patriotic Front (RPF-Inkotanyi), kimemteua rasmi Rais aliye madarakani Paul Kagame kuwa mgombea urais wake kwa ajili ya uchaguzi ujao wa urais utakaofanyika mwezi Julai.
Rais Kagame amechaguliwa kwa asilimia 99.1 ya kura wakati wa mkutano wa chama hicho, uliofanyika Jumamosi mjini Kigali.
Katika hotuba yake ya kukubali kuteuliwa, Rais Kagame ametoa shukrani kwa imani aliyopewa ya kuendelea kuijenga nchi. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwaandaa viongozi wa kizazi kijacho ndani ya chama, akiwataka wanachama kufikiria zaidi ya enzi zao na kuzingatia uongozi wa baadaye wa RPF-Inkotanyi.
Chama hicho pia kilitangaza orodha ya wagombea 70 wa ubunge na ilani yake ya miaka mitano ijayo kama kitakaposhinda uchaguzi. Mkutano wa chama hicho unafuatia chaguzi za mchujo za vyama zilizofanyika mwezi Februari ili kuwachagua watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi ujao wa rais na wabunge utakaoifanyika Julai 15.