Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry alitangaza mapema Jumanne kwamba atajiuzulu mara tu baraza la mpito la rais litakapoundwa, akifuata shinikizo la kimataifa linalotaka kuokoa nchi hiyo inayolemewa na magenge ya kikatili ambayo baadhi ya wataalam wanasema yameanzisha vita vya chini vya wenyewe kwa wenyewe.
Henry alitoa tangazo hilo saa chache baada ya maafisa wakiwemo viongozi wa Karibiani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana nchini Jamaica ili kujadili kwa haraka suluhu la kusitisha mgogoro unaoendelea nchini Haiti.
Henry ameshindwa kuingia Haiti kwa sababu ghasia zilifunga viwanja vyake vya ndege vya kimataifa. Alikuwa amewasili Puerto Rico wiki moja iliyopita, baada ya kuzuiwa kutua katika Jamhuri ya Dominika, ambapo maafisa walisema hakuwa na mpango wa ndege unaohitajika. Maafisa wa Dominika pia walifunga anga kwa safari za ndege kwenda na kutoka Haiti.
Haijabainika mara moja ni nani hasa angeiongoza Haiti kutoka katika mzozo huo ambapo magenge yenye silaha nzito yameteketeza vituo vya polisi, kushambulia uwanja mkuu wa ndege na kuvamia magereza makubwa mawili ya nchi hiyo. Uvamizi huo ulisababisha kuachiliwa kwa wafungwa zaidi ya 4,000.