Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekosoa mswada wa bunge wa kulazimisha kampuni mama ya TikTok kuuza programu hiyo au ipigwe marufuku nchini Marekani.
Bw Trump, ambaye alijaribu kupiga marufuku TikTok mnamo 2020 akiwa katika Ikulu ya White House, alisema pendekezo hilo litatengeneza fursa ya kutoa faida kwa mmiliki wa Facebook Meta bila usawa wa haki.
Wabunge wanajadili hatua ambayo italazimisha kampuni mama ya TikTok ByteDance kuiuza ifikapo tarehe 30 Septemba.
Rais Joe Biden amesema atatia saini mswada huo iwapo utapitishwa.
“Bila TikTok, unaweza kuifanya Facebook kuwa kubwa zaidi, na ninaichukulia Facebook kuwa adui wa watu,” Bw Trump aliambia NBC Jumatatu.
Alipoulizwa kuhusu usalama wa programu, mgombea urais wa Republican alisema “kuna mengi mazuri na kuna mengi mabaya” kwenye mtandao wa kijamii.
“Kuna watu wengi kwenye TikTok wanaoipenda. Kuna watoto wengi wachanga kwenye TikTok ambao watachanganyikiwa bila hiyo,” Bw Trump aliongeza.
Jumuiya ya kijasusi ya Marekani imeonya kuwa serikali ya China inatumia TikTok katika majaribio ya kutilia shaka uongozi wa Marekani na kudhoofisha demokrasia.
Katika ripoti ya kila mwaka kuhusu vitisho kwa usalama wa Marekani, iliyotolewa Jumatatu, Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa iliandika kwamba akaunti za TikTok kutoka kwa kitengo cha propaganda za serikali ya China “ziliripotiwa kuwalenga wagombea kutoka vyama vyote viwili vya siasa wakati wa uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka 2022”.