India imetangaza sheria zitakazoiruhusu kutekeleza mswada wenye utata wa uraia unaowatenga Waislamu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya India ilitangaza sheria hizo Jumatatu, kabla ya uchaguzi mkuu wa India huku Waziri Mkuu Narendra Modi akitajwa kuwa atawania muhula adimu wa tatu madarakani.
Sheria ya Uraia (Marekebisho) inatoa njia ya haraka ya uraia kwa wahamiaji kutoka Afghanistan, Bangladesh, na Pakistani – ambao si Waislamu.
Sheria hiyo tata itatumika kwa walio wachache wa kidini wanaoteswa kwa misingi ya kidini, wakiwemo Wahindu, Masingasinga, Wabudha, Wajaini, Waparsi na Wakristo.
Hatua hiyo ambayo upinzani na wakosoaji wameichukulia kama inayopinga Waislamu, itakuwa mabadiliko ya kwanza ya uraia katika katiba ya India ambayo inakataza ubaguzi kwa misingi ya kidini.
Muswada huo, uliopitishwa na bunge la India mnamo 2019, haukuweza kuanza kutumika hadi sheria hizo zifahamishwe.
Licha ya kupokelewa vyema na Modi, mzalendo wa Kihindu, mswada huo ulipingwa vikali na vyama vya upinzani, ambavyo vilidai kuwa ni kinyume cha sheria na kuwatenga Waislamu wa India milioni 200.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Amit Shah alimsifu Modi Jumatatu jioni, akisema “alitimiza ahadi nyingine na akatambua ahadi ya watunga katiba yetu kwa Wahindu, Masingasinga, Wabudha, Wajaini, Waparsi na Wakristo wanaoishi katika nchi hizo” katika chapisho X.