Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Shirika la Community Led Initiative for Women (CLIW) wanayo furaha kubwa kutangaza uzinduzi wa mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni, ukiwa na lengo la kuchangia juhudu za serikali katika kutekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuharakisha Hatua na Uwekezaji kwa Afya na Ustawi wa Vijana 2021/22 – 2024/25 (NAIA-AHW).
Mradi huu utachangia afua kuu Nne kati ya afua sita: (1) Kuzuia VVU; (2) Kuzuia mimba za Ujana; (3) Kuzuia Ukatili wa Kijinsia, Kimwili na Kihisia; (4) Kuboresha Lishe; Kukuza Ujuzi na kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana wanaoishia na virusi vya ukimwi.
Afua hizo zinaainisha maeneo ya kipaumbele ya uwekezaji ambayo yanaweza kuhakikisha kundi lenye tija na, hatimaye, taifa lenye tija.
Pia mradi utachangia dhamira ya Tanzania katika utekelezaji wa Azimio la Umoja la Umoja wa Mataifa kuhusu VVU na UKIMWI la mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu na Agenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063, ilikuwezesha Tanzania kufanikisha malengo kwa mujibu wa taratibu na kanuni bora za kitaifa na Kimataifa. Tanzania imelenga kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kitaifa la 95-95-95 (Asilimia 95 ya wanaoishi na VVU watambue hali zao, asilimia 95 ya WAVIU wawe wameanza dawa za kupunguza makali ya VVU na asilimia 95 ya walioanza dawa wapunguzwe kiwango cha virusimwilini) ifikapo mwaka 2030.
Lengo kuu la mradi huu ni kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake vijana, hasa wale walio katika mazingira hatarishi kama vile wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au wanaofanya kazi katika mazingira yenye hatari ya kuambukizwa VVU, wanapata uelewa na ujuzi wa kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU. Kupitia mradi huu, tunalenga kuhamasisha upimaji wa VVU, upatikanaji wa huduma za afya bora na salama, na matumizi sahihi ya dawa za kujilinda na kupunguza makali ya VVU.
Wanufaika wa mradi huu ni wasichana na wanawake vijana wenye umri kati ya miaka 17-25 wanaoishi au walio hatarini kupata maambukizi ya VVU katika Wilaya ya Kinondoni.
Kwa kufanikisha malengo ya mradi huu, CDF na CLIW watatekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa vijana hawa juu ya kujitambua, kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU, ushauri nasaha, upimaji, na matumizi sahihi ya dawa za kujilinda na kupunguza makali ya VVU. Vijana hawa watapewa ujuzi na kisha kufanya kazi ya kuelimisha wenzao katika jamii kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mijadala, midahalo na vipeperushi vyenye jumbe mbalimbali.
Aidha, kupitia mradi huu, wahudumu wa afya watapatiwa mafunzo na ujuzi wa kutoa huduma bora na rafiki kwa wasichana na wanawake vijana wanaoishi au walio hatarini kupata maambukizi ya VVU ili kupunguza maambukizi ya VVU.
Tunaamini kuwa mradi huu utachangia kujenga uelewa zaidi miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na kutafuta huduma za afya bora. Tunatoa wito kwa jamii na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo ya mradi huu muhimu.