Polisi wa Zimbabwe siku ya Jumatano walisema wamemkamata mwanamume anayedai kuwa nabii wa dhehebu la mitume katika madhabahu ambapo waumini wanakaa katika boma na mamlaka ilikuta makaburi 16 ambayo hayajasajiliwa, yakiwemo ya watoto wachanga, na zaidi ya watoto 250 wakitumika kama vibarua nafuu.
Katika taarifa yake, msemaji wa polisi Paul Nyathi alisema Ishmael Chokurongerwa, 56, “aliyejiita nabii”, aliongoza dhehebu lenye waumini zaidi ya 1,000 katika shamba lililo umbali wa kilomita 34 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu, Harare, ambako watoto walikuwa wakikaa pamoja na waumini wengine.
Watoto hao “walikuwa wakitumiwa kufanya shughuli mbalimbali za kimwili kwa manufaa ya uongozi wa madhehebu,” alisema. Kati ya watoto 251, 246 hawakuwa na vyeti vya kuzaliwa.
“Polisi walibaini kuwa watoto wote wa umri wa kwenda shule hawakuhudhuria elimu rasmi na walinyanyaswa kama kazi ya bei nafuu, wakifanya kazi za mikono kwa jina la kufundishwa stadi za maisha,” alisema Nyathi.