Jeshi la polisi wilaya ya Tanga limeishukuru serikali ya Uswisi kwa kuwaletea mradi wa Elimu ya usalama barabara kwa bodaboda ambao utaweza kumaliza changamoto za makosa ya usalama wa barabara.
Akiongea wakati wa mafunzo ya usalama wa barabara kwa madereva wa bodaboda wa kata ya Magaoni Jijini Tanga Mkuu wa usalama wa barabara wilaya ya Tanga amesema kuwa mafunzo hayo yataweza kusaidia makosa ya barabara kwa kiwango kikubwa Kwa madereva hao.
Alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya makosa ya barabara yanayofanywa na madereva wa bodaboda ambayo wakati mwingine yanasababisha uvunjifu wa amani ni inatokana na kukosa uwelewa wa sheria.
“Kupitia mafunzo hayo tumewapa elimu ya kuwataka wajiepushe na makosa ya kujichukulia sheria mkononi pale ambapo wanapopata ajali hivyo tumewataka wajiepushe na masuala ya uhalifu pindi inapotokea ajali”alisema Mkuu huyo wa usalama barabara
Aidha Afisa Miradi Mwandamizi Mratibu kutoka Taasisi ya Amend Ramadhani Nyaza alisema kuwa mpaka Sasa wameweza kuwafikia madereva bodaboda 180 wakiwa na lengo la kufikia madereva 500.
“Mradi huu ambao unafadhiliwa na ubalozi wa Uswizi unalengo la kuwafikia vijana 750 wanaofanya shughuli za usafirishaji kwa kutumia bodaboda katika mikoa ya Tanga na Dodoma”alisema Nyanza.
Nae Diwani kata ya Mabawa Athumani Babu alisema kuwa mradi huo wa Elimu utaweza kusaidia kupunguza changamoto ya ajali za barabara kwenye maeneo mbalimbali Jiji Tanga.
Hata hivyo madereva wa bodaboda waliopatiwa mafunzo walisema kuwa wataweza kuwakuwa mabalozi Wazuri wa kuendeleleza elimu hiyo Kwa wenzao Ili kupunguza changamoto ya uwepo wa ajali za barabara.
“Tunakwenda kuacha kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia shughuli zetu za bodaboda lakini na kuwashawishi wenzetu wengine kuachana na tabia za kujichukulia sheria mkononi lakini na kufuata sheria za usalama barabara “alisema Nasib Issa dereva wa bodaboda