Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wageni wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais William Ruto wa Kenya walipowasili Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 14 Machi, 2024.
Kwenye mazungumzo yao wamezungumzia masuala ya mtangamano wa Afrika Mashariki hususan umuhimu wa kuharakisha zoezi la kukusanya maoni ya Wananchi Juu ya muundo na maeneo ya kuangaliwa katika Rasimu ya Katiba ya Fungamano la kisiasa la Afrika Mashariki (EAC Political Confederation).
Zoezi hilo limeshafanyika katika nchi za Burundi, Uganda na Kenya na linatekelezwa na Timu ya Wataalamu inayoundwa na Wajumbe watatu kutoka kila nchi Mwanachama.
Mkutano kati ya marais hao unaenda sambamba na mkutano wa Machi 14, 1996 wa Marais Daniel Arap Moi, Yoweri Museveni na Benjamin Mkapa ambao, uliweka msingi wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Shirikisho la Kisiasa litakapoundwa litajengwa katika mihimili mitatu; sera za pamoja za mambo ya nje na usalama, utawala bora na utekelezaji madhubuti.