Wafuasi wa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko, waliingia kwenye mitaa ya Dakar mapema Ijumaa kufuatia kuachiliwa kwake kutoka jela mwishoni mwa Alhamisi, kabla ya uchaguzi wa urais baadaye mwezi huu.
Sonko anaonekana sana kama mpinzani mkuu wa chama tawala cha Rais Macky Sall. Alipokelewa nje ya gereza na umati wa wafuasi wake wakipeperusha bendera, wakiimba na kuinua mabango.
Sonko alikuwa gerezani tangu Julai na amepigana vita vya muda mrefu vya kisheria kuwania urais katika uchaguzi wa Machi 24. Sonko na mshirika wake mkuu, Bassirou Diomaye Faye, wote waliachiliwa, wakili wake Bamba Cisse aliambia The Associated Press.
Haikuwa wazi mara moja jinsi kutolewa kwao kungeathiri uchaguzi. Faye aliteuliwa kuwa mgombeaji wa uchaguzi wa upinzani baada ya Sonko kuzuiwa kuwania.
Wafuasi pia walikusanyika katika nyumba ya Sonko na katika maeneo mengine mjini Dakar kusherehekea. Misafara ya wafuasi ilizunguka mji mkuu wakipiga honi na kupiga kelele hadi usiku sana.