Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Chrysoula Zacharopoulou, Waziri wa Nchi-Maendeleo ya Uchumi (Secretary of State for Economic Development) wa Ufaransa.
Akizungumza malengo na dhamira ya kutoa mualiko kwa Wizara ya Maji Tanzania, Mheshimiwa Chrysoula amesema Serikali ya Ufaransa inatambua na kuthamini jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika dhamira ya kuimarisha huduma ya Maji kwa wananchi na kwamba wanaamini hiki ni kipaumbele chake katika kipindi cha uongozi wake na kusisitiza kwamba katika kuunga mkono jitihada hizo serikali yake ya awamu ya sita Serikali ya Ufaransa imejidhatiti kuwekeza katika miradi ya Maji mingi zaidi kwa kuthamini kazi anayoifanya na pia umuhimu wa sekta kwa maisha ya watu kwani maji ni uhai.
Pia, Kiongozi huyo ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa serikali yake kukamilisha Miradi ya Maji Mikubwa na ya Kimkakati na usimamizi mzuri wenye kujali thamani ya fedha na wakati katika pamoja na Miradi ile inayoendelea ambayo inatekelezwa kwa Mashirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo Ufaransa AFD kama Miradi ya Maji miji ya SHINYANGA, MUSOMA, BUKOBA, MWANZA AWAMU YA 1 na MOROGORO AWAMU YA 1 pamoja na Mradi wa Majitaka eneo la Kurasini Jijini DAR ES SALAAM inayofadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo Ufaransa(AFD).