Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu ameliamrisha jeshi la nchi hiyo kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola wahusika wa mauaji ya wanajeshi 16 wa nchi hiyo katika jimbo la kusini la Delta.
Rais Tinubu pia amelaani vikali shambulio hilo lililopelekea kuuawa wanajeshi 16 wa nchi hiyo wakiwemo mameja wawili na kapteni mmoja na kusisitiza kuwa, hujuma hiyo ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya taifa.
“Waliotekeleza jinai hii ya kioga na kihaini lazima watawajibishwa na kuadhibiwa,”ameeleza Rais wa Nigeria ambaye aliahidi kukabiliana na changamoto za usalama nchini humo tangu aingie madarakani.
Amesema: Nimetoa ridhaa na mamlaka kamili kwa makao makuu ya Wizara ya Ulinzi na mkuu wa majeshi, ili kuhakikisha kuwa askari waliouawa na raia ambao ni wahanga wa shambulio hilo wanapata haki.
Rais wa Nigeria amesema uchunguzi unaoendelea umepelekea kutiwa mbaroni watu kadhaa wanaohusishwa na shambulio hilo la Jumamosi iliyopita katika jimbo la kusini la Delta.