Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa ameielekeza Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) kufikia mwezi Oktoba 2024 iwe imempata mwekezaji binafsi ambaye ni mtoa huduma wa mabasi hayo ili kuleta ufanisi.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akiwasilisha Randama ya Bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI Fungu namba 56 na Fungu namba 2 la Tume ya Utumishi wa Walimu mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ukumbi wa Anne Makinda uliopo bungeni jijini Dodoma.
Akisisitiza hilo Mhe. Mchengerwa amesema kuwepo kwa mwekezaji binafisi katika mradi huo utaendeshwa kwa ufanisi kutokana na kulipa kodi kwa serikali na wakati huohuo atawajibika endapo atatoa huduma isiyostahili.
“Atahakikisha anatoa huduma nzuri ili watu waweze kuhudumiwa na kama tukileta mabasi ya kutosha watu wa Dar es Salaam watapaki mabasi yao watatumia mwendokasi na tutakwenda kuokoa zaidi ya sh.bilioni 300 ambayo tungeitumia kununua mabasi” amesema Mohammed Mchengerwa
Hata hivyo Mhe. Mchengerwa amesema ifikapo mwezi Septemba hadi Oktoba serikali itakuwa imepata mabasi ya kutosha ya kuendesha njia zote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi ili watanzania wa Dar es Salaam waweze kuhudumiwa vizuri kabla ya kuanza kupeleka huduma ya mwendokasi katika majiji mengine.