Shirika la Kimataifa la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, linaripoti kwamba idadi ya watu wanaolazimishwa kufanya kazi kinyume na matakwa yao imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni na kufikia wastani ya watu milioni 27.6 kwa siku.
Kulingana na takwimu mpya, miongoni mwa watu hao milioni 27.6 waloorodheshwa mwaka 2021, ni wale ambao wako katika utumwa wa mambo leo, kukiwepo zaidi ya watoto milioni 3.3 pamoja na milioni 22 wanaolazimishwa kuolewa.
Aidha, utafiti wa ripoti hiyo ya ILO iliyotangazwa Jumanne unaonesha kwamba, watu hao wanaofanyishwa kazi kwa lazima wamezalisha karibu dola billion 236 za faida haramu kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko kubwa la dola bilioni 64 tangu mwaka 2014.
Utafiti huo imesema ongezeko hilo linatokana na ongezeko la watu wanaolazimishwa kufanya kazi na uwiyano kati ya viwango vya juu vya dhulma na faid zilizokithiri.
Wasafirishaji haramu wa binadamu na wahalifu waowatumia wafanyakazi kwa nguvu wanajipatia karibu dola 10,000 kutoka kila muathirika.
Utafiti huo umegundua kwamba mtindo uloenea zaidi wa kazi za lazima ni biashara haramu ya ngono.
Ingawa inawakilisha asilimia 27 ya waathirika wote wa kazi za kulazimishwa, lakini ukandamizaji wa kijinsia inaingiza asilimia 73 ya jumla ya faida haramu inayopatikana.
Kulingana na VOA takribani waathirika wanne kati ya watano ni wasichana na wanawake, Shirika hilo la Kazi la Umoja wa Mataifa limesema, ambapo zaidi ya robo ya visa vyote vinawahusu watoto.
ILO, imeripoti kuwa inakadiriwa asilimia 85 ya waloathiriwa kwa kufanyishwa kazi kwa lazima ni pamoja na wale wanaofanyishwa kazi “kwaajili ya watu binafsi,” inayojumuisha tabia kama vile utumwa, utwana, kufanya kazi ili kulipa deni na aina kadhaa za ombaomba ili mapato yanamnufaisha mtu mwengine.