Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (LATRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu juu ya madhara ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu kwa madereva bodaboda na bajaji zaidi ya 200 wa Wilaya ya Arusha.
Aidha, madereva hao wa Bajaji na Bodaboda wameahidi watakuwa mabalozi wazuri wa kupinga dawa za kulevya na kufikisha elimu juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya kwa madereva wenzao na jamii kwa ujumla.
Akiongea wakati akitoa mada katika kikao cha wadau wa usafirishaji kilichofanyika Jijini Arusha Afisa wa Mafunzo na Elimu wa Mamlaka DCEA Shabani Miraji amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu kuhakikisha matumizi ya dawa za kulevya nchini yanapigwa vita kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali.
Amesema kwamba wasafirishaji hao ni sehemu muhimu ndio maana wamekuwa wakiwapa Elimu ya mara kwa mara kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inakuwa historia ambapo wadau hao wakishirikishwa vyema kutoa elimu ya udhibiti na matumizi ya dawa hizo Zoezi hilo litakuwa rahisi kudhibiti usafirishaji na matumizi.
Awali akiongea mara baada ya kikao hicho Afisa udhibiti wa Kemikali bashirifu kanda ya kaskazini Thomas Muhesa ameeleza kwamba wamekutana na kundi Kubwa ambao wanatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo mbalimbali kutoka sehemu Moja kwenda nyingine.