Shirika la Taifa la Mafuta la Libya (NOC) limesema kwenye ripoti yake ya jana Jumanne kwamba nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ilizalisha zaidi ya mapipa milioni 33.5 ya mafuta ghafi mwezi uliopita wa Februari.
Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook imesema kuwa, mwezi uliopita Libya ilizalisha tani 515,461 za mafuta ya petroli na tani 110,729 za kemikali za petroli.
Mafuta na gesi ni bidhaa zinazochukua nafasi muhimu katika uchumi wa Libya, kwani nchi hiyo ina akiba kubwa sana ya mafuta barani Afrika.
Hata hivyo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na vita vya silaha na mashambulizi dhidi ya sekta ya uzalishaji na usafirishaji mafuta.
Wakati wa mkutano wa kumi wa kawaida wa Baraza Kuu la Nishati na Maji uliofanyika Jumatatu, Mwenyekiti wa NOC Farhat Ben Gadara alisema kuwa uzalishaji wa mafuta wa kila siku nchini Libya utazidi mapipa milioni 1.5 ifikapo mwisho wa 2025, na mapipa milioni 2 ndani ya miaka 3, akielezea kuwa, kiwango hicho kinahitaji ukaguzi wa kudumu wa fedha.