Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kwamba limeomba kupatiwa dola milioni 189.1 za Kimarekani ili kuongeza misaada yake kwa watoto waliokimbia makazi yao na familia zilizoko kwenye mazingira magumu nchini Somalia mwaka 2024.
UNICEF imesema, wafadhili wametoa dola milioni 4.9 kufikia mwezi Februari kwa ajili ya kuzuia kipindupindu na utapiamlo, kupunguza na kukabiliana na hali hiyo, usambazaji wa maji, usafi wa mazingira, ulinzi wa watoto, kutoa elimu katika mazingira ya dharura, chanjo, kuzuia unyanyasaji wa kingono na kuwasaidia ipasavyo watu walioathirika.
Kwa mujibu wa UNICEF, watoto nchini Somalia wako katika hatari ya mafuriko makubwa, ikiwa ni pamoja na mafuriko ya mito, wakati wa sehemu ya kwanza ya msimu wa mvua wa Gu 2024 ambao huanzia mwezi Machi hadi mmwanzoni mwa Aprili, huku tukio la El Nino nalo likitabiriwa kuendelea.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, takriban watoto 68,676, ambapo kati yao wasichana ni 31,775 walioathiriwa na hali za dharura, hivi sasa wamepata nafasi za kupewa elimu kwa muda katika wilaya 12 zilizoathiriwa na maafa nchini Somalia.