Polisi wa Brazil wamependekeza Jair Bolsonaro ashtakiwe kwa kughushi cheti chake cha chanjo ya COVID.
Shtaka la polisi wa shirikisho lilitolewa na Mahakama ya Juu ya Brazil Jumanne, kufuatia uchunguzi ulioanza mwaka jana.
Uchunguzi huo ni mojawapo ya kesi kadhaa ambazo mwanasiasa huyo wa siasa kali za mrengo wa kulia anakabiliwa na muhula wake wa uongozi uliomalizika Desemba 2022.
Bolsonaro alikuwa ameonyesha kupinga chanjo ya COVID-19 huku pia akipuuza athari za kiafya za virusi hivyo na ukali wa janga hilo.
Sasa ni juu ya mwendesha-mashtaka mkuu wa Brazili kuamua iwapo atamfungulia mashtaka Bolsonaro katika Mahakama ya Juu Zaidi ya Brazil.
Wakili wa Bolsonaro, Fabio Wajngarten, alikanusha madai ya polisi kama “upuuzi.”
“Wakati alipokuwa rais, [Bolsonaro] hakuruhusiwa kuwasilisha aina yoyote ya cheti katika safari zake,” Wajngarten alisema, huku akilaani “mateso ya kisiasa” dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa Brazil.