Jeshi la Israel lilisema siku ya Jumatano kuwa limewaua takriban watu 90 wenye silaha na kuwakamata 160 katika uvamizi katika hospitali ya Al Shifa huko Gaza.
Al Shifa, hospitali kubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza kabla ya vita, sasa ni moja ya vituo vichache vya huduma za afya ambavyo vinafanya kazi kwa sehemu kaskazini mwa eneo hilo, na pia imekuwa makazi ya raia waliohamishwa.
“Katika siku iliyopita, wanajeshi wamewaondoa magaidi na kupata silaha katika eneo la hospitali, huku wakizuia madhara kwa raia, wagonjwa, timu za matibabu na vifaa vya matibabu,” jeshi lilisema katika taarifa.
Uvamizi wa Israeli katika hospitali hiyo ulianza mapema Jumatatu. Jeshi lilisema lilituma vikosi maalum vinavyoungwa mkono na askari wa miguu na vifaru, kulingana na kijasusi kwamba hospitali hiyo ilikuwa inatumiwa tena na watu wenye silaha.