Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amezindua Kamati ya Kupitia Majukumu na Maboresho ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim zamani Chuo cha Diplomasia.
Akizindua Kamati hiyo leo tarahe 20 Machi 2024 jijini Dar es Salaam, Mhe. Makamba amesema kazi kubwa ya kamati hiyo pamoja na mambo mengine ni kufanya tathmini na kuanisha maeneo yanayohitaji maboresho ili kuwa na kituo chenye kukidhi mahitaji ya wadau wake kwa mahitaji ya sasa na ya kizazi kijacho.
Amesema hatua hiyo inatokana na mapendekezo ya kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya Tathmni ya Utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ikiwemo Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim.
Kuhusu Kituo hicho, pamoja na mambo mengine kamati hiyo iliyoundwa na Mhe. Rais ilipendekeza umuhimu wa kufanyika tathmini ya kina na kufanya mabadiliko ili kuwa na Taasisi ya Mafunzo ya Kitaaluma, Utafiti na Stadi za Kidiplomasia na pia kuwa Kituo rejea cha fikra (Think Tank).
“Katika kutekeleza ushauri na mapendekezo ya Kamati, Wizara imechukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hiyo ni mimi kama Waziri mwenye dhamana kuona ni vyema nikateua Timu ndogo ya Wabobezi watakaofanya tathmini ya kina katika majukumu ya Kituo na kuainisha maeneo yanayohitaji maboresho ili kuwa na Kituo Mahiri chenye kukidhi mahitaji ya wadau wake kwa mahitaji ya sasa na ya kizazi kijacho,” alisisitiza Waziri Makamba.
Kadhalika Kituo cha Dkt. Salim tayari kimesaini Hati za Makubaliano na Taasisi kutoka nchi za Algeria, Angola, Afrika Kusini na Umoja wa Falme za Kiarabu. Kituo pia kimeingia makubaliano na Chuo cha Usimamizi wa Mahakama, Benki Kuu ya Tanzania, Chuo cha Utawala wa Umma, Chuo cha Taifa cha Ulinzi na Mpango wa Hiyari wa Afrika wa Kujitathmini kwa vigezo vya Utawala Bora(APRM) ambapo kamati hii itaangalia utekelezaji wa Hati hizo za Makubaliano na kuanisha maeneo ambayo yanahitaji msukumo na maboresho ili kuleta manufaa yaliyokusidiwa.
Kamati hii ina jumla ya wajumbe nane ikiongozwa na Mwenyekiti Bal. Khamis S. Kagasheki na wajumbe wengine ni pamoja na Bal. Dkt. Ramadhan Dau, Dkt. Salim O. Hamad, Prof. Marcellina M. Chijoriga, Dkt. Lucy Shule, Dkt. Godfrey Sansa, Dkt. Kadari Singo, na Dkt. Asumpta Muna
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati, Bal. Kagasheki amesema kamati itasimamia vyema majukumu iliyopewa na kupendekeza pale itapoona uhutaji wenye tija zaidi hata ya majukumu vipengele vya sasa.
Awali Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilijulikana kama Kituo cha Mahusiano ya Kigeni cha Msumbiji na Tanzania, au Kituo cha Mahusiano ya Kigeni (CFR).