Takriban watu 65 walikufa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, Wizara ya Afya ya eneo hilo imesema leo, na kufanya jumla ya waliouawa tangu Israel ilipoanzisha kampeni yake ya kijeshi kufuatia shambulio la kigaidi la Hamas Oktoba 7 kufikia 31,988.
Imeongeza kuwa zaidi ya watu 74,000 wamejeruhiwa.
Miili mingi zaidi inadhaniwa kuwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya watatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano endelevu huko Gaza katika mkutano wao wa kilele mjini Brussels ,mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Josep Borrell amesema leo.
“Leo Baraza linakwenda mbali zaidi” kuliko miezi iliyopita, alisema kabla ya mkutano huo. “Kuomba kusitishwa kwa mapigano endelevu, bila shaka kuuliza pia uhuru wa mateka, lakini kuonyesha wasiwasi mkubwa kwa hali ya watu wa Gaza, ambayo haikubaliki.”