Mazungumzo ya kuunda baraza tawala la mpito nchini Haiti yaliendelea jana Jumatano wakati Marekani ikiwahamisha kwa ndege raia zaidi.
Marekani imewapeleka raia wake sehemu salama zaidi kufuatia machafuko ya magenge ya uhalifu yaliyolikumba taifa hilo.
Balozi wa Guyana kwenye Umoja wa Mataifa Carolyn Rodrigues-Birkett amesema majadiliano bado yanaendelea na pengine yatachukua muda mrefu, ingawa amesema hatua zinapigwa.
Duru za serikali ya Haiti zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba hata majina ya wajumbe wa baraza hilo bado hayajawasilishwa kwa Waziri Mkuu anayeondoka Ariel Henry.
Baraza hilo linatarajiwa kumteua Waziri Mkuu wa mpito atakayesimamia uchaguzi wa kwanza wa taifa hilo tangu mwaka 2016.
Mji mkuu wa Haiti umekuwa chini ya makundi yaliyojihami kwa silaha kwa wiki kadhaa sasa, huku vituo vingi vya polisi, vituo vya kusambaza umeme, majengo ya umaa na miundombinu vikishambuliwa na miili ya waliouawa ikiwa imezagaa barabarani.