Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma imekagua na kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la DAWASA Yetu lililogharimu shilingi bilioni 48.9 na linatarajiwa kukamilika mwezi June mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mradi wa jengo hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deus Sangu amesema kuwa Kamati imejionea utekelezaji mzuri wa mradi huu wa ujenzi wa jengo kwa ufanisi na kwa ubora.
Amesema kuwa kupitia jengo hili, DAWASA ambayo ni Mamlaka kubwa nchini ya maji litasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.
Mhe. Sangu ameipongeza Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia umuhimu wa kazi kubwa waliyonayo DAWASA ya kuhudumia majimbo 16 ya uchaguzi na mikoa minne ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, baadhi ya maeneo ya Morogoro na Tanga, na kuamua kutoa fedha za kujenga jengo hili la kisasa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Ndugu Laston Msongole ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kutembelea mradi huu na kujionea maendeleo ya jengo letu na hatua ilipofikia.
“Wamejionea na wameridhika na kazi iliyofanyika pamoja na kuona thamani ya fedha iliyowekweza imeleta tija, tunawaahidi kukamilisha sehemu iliyobaki ndani ya wakati,” ameeleza Ndugu Msongole.