Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesisitiza suala la kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.
Dkt. Biteko amesisitiza hilo leo Machi 25,2024 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi nchini Tanzania.
Aidha ufunguzi huo umeambatana na uzinduzi wa namba namba 115 ya kuwasiliana na watoa huduma kupitia mfumo wa M-mama unaoratibiwa katika hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo kwa ambapo kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.
“Napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo wa ‘Touch Health’ na ‘Pathfinder International’ kwa mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa wote,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Sambamba na hilo ameagiza kuwekwa Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa huku akiongeza kuwa miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.