Watu kadhaa wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko kusini mwa Liberia.
Waziri wa Madini wa Liberia, Wilmot Paye jana Jumanne alithibitisha habari ya kutokea ajali hiyo na kuongeza kuwa, takwimu za awali zinaonesha kuwa watu wasiopungua saba wameaga dunia kwenye mkasa huo uliotokea usiku wa kuamkia jana.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, huenda idadi hiyo ikaongezeka, na kwamba tayari timu ya maafisa wa serikali imetumwa katika eneo la tukio katika Kaunti ya River Cess.
Paye amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mkasa huo unaendelea, akisistiza kuwa serikali itaiwajibisha na kuibebesha dhima kampuni iliyokuwa inaendeleza uchimbaji wa madini katika eneo hilo kinyume cha sheria.
Shirika la habari la Reuters limenukuu mashuhuda na duru za habari zinazosema, makumi ya wachimba migodi wamepoteza maisha katika ajali hiyo.