Wabunge wa Togo jana walipitisha katiba mpya na kuiondoa nchi hiyo kutoka muundo wa urais hadi bunge na kisha kulipatia bunge mamlaka ya kumchagua rais wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika.
Katiba mpya ya Togo inaeleza kuwa Rais wa nchi hiyo atachaguliwa na bunge ‘bila ya mjadala bungeni’ ili kuiongoza nchi kwa muhula mmoja wa miaka sita, na hatachaguliwa na wananchi.
Wabunge wa Togo wameifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ikiwa ni chini ya mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi ujao wa bunge uliokuwa umepangwa kufanyika hapo awali; hata hivyo bado haijajulikana ni lini mabadiliko hayo ambayo yamepasishwa kwa kura 89 za ndio, moja ya kupinga, na moja ya kujizuia yataanza kutekelezwa.
Awali Rais wa Togo alikuwa akisalia madarakani kwa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja. Mabadiliko haya tajwa ya katiba, yaliyopendekezwa na kundi la wabunge, wengi wao wakiwa ni kutoka chama tawala cha Togo cha Union for the Republic (UNIR) yamepasishwa kwa kura nyingi.
Katiba mpya ya Togo pia imeanzisha cheo cha Mkuu wa Baraza la Mawaziri atakayekuwa na mamlaka kamili ya kusimamia shughuli za serikali na kuwajibika ipasavyo.