Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka waganga wafawidhi nchini na Watumishi ndani ya Sekta ya Afya kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya.
Pia amesema sekta binafsi imesaidia kwa kiwango kikubwa kuipunguzia Serikali mzigo hasa upande wa ajira kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia sekta binafsi, hali ambayo sio rahisi kuiachia mzigo serikali pekee.
Dtk. Mollel ameyasema hayo Machi 27,2024 wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki na kuchangia mada zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo.
Dkt. Mollel amewaasa Wakurugenzi wa OR- TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuhakikisha vinapata vituo hivyo mapema iwezekanavyo.
“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mambo mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja, nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati”, amesema Mollel na kuongeza .
“Tunataka tutakapokutana tena katika mkutano wa mwaka 2026 tutazungumza masula mengine kama kuajiri watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuongezwa” amesisitiza Mollel.
Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.