Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kutokana na ongezeko la hatari kwa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh mjini Geneva, Uswisi, imesema: “Miaka miwili ya mizozo katika maeneo ya Kivu Kaskazini huko Rutshuru na Masisi imewalazimisha zaidi ya watu milioni 1.3 kukimbia makazi yao ndani ya DRC, na kusababisha jumla ya watu milioni 5.7 kuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.”
Ameongeza kuwa tangu mapigano makali yashike kasi katika mji wa Sake, tarehe 7 Februari, karibu watu 300,000 wamewasili katika jiji la Goma, ambako hali ilikuwa mbaya.
Watu zaidi ya 85,000 walikuwa wamekimbia ghasia hizo hizo na kutafuta makazi katika eneo la Minova la Kivu Kusini, ambalo tayari lilikuwa limepokea watu 156,000 waliokimbia makazi yao tangu Januari.