Serikali Mkoani Geita imekiagiza Chama cha Ushirika wilaya ya Geita (GCU), Mrajisi Msaidizi wa Mkoa Pamoja na Maafisa Kilimo kuhakikisha wanashirikiana katika kufufua viwanda chakavu viwili ambavyo hapo mwanzo vilikiwa vikitumika kuchakata Mafuta ya Alizeti pamoja na Pamba.
Akitoa Maagizo hayo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita , Bi. Grace Kingalame katika Mkutano wa 6 wa chama cha Ushirika kilichofanyika Mjini Geita Kingalame amesema ufufuaji wa viwanda hivyo utasaidia chama cha Ushirika kujisimamia pamoja na Mkombozi kwa wakulima katika kuuza pamba kwa bei rafiki.
“Mkutano huu uwe ni sehemu ya utekelezaji wa Mikakati tuliyojiwekea kama Mkoa ya uimarishaji wa Ushirika hapa Mkoani kwetu Geita tunaamini ufufuaji wa kiwanda cha kuchambua pamba na kusindika mafuta vilivyopo hapa kasamwa vinavyomilikiwa na GCU limited ndivyo mkombozi wa Pekee kwa mkulima katika kuuza pamba yake kwa bei nzuri , ” Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Kingalame.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wilaya ya Geita Bi. Zainabu Shabani amesema tayari wametenga kiasi cha Fedha shilingi Bilioni 6 kwa ajili ya ukarabati wa viwanda hivyo viwili ambavyo vitakuwa mkombozi kwa wakulima wa Mkoa wa Geita.
“Tumetenga kiasi cha Bilioni 6 ambayo itapitishwa kwenye haya makisio bilioni 6 kufufua viwanda vyote viwili pamoja na Fedha ya Kununulia Mazao , ” Bi. Zainabu .
Katika hatua nyingine Bi. Zainabu amesema wamepokea maagizo yote yaliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita na kusema watakwenda kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kila sehemu yenye changamoto inatatuliwa kupitia vyama vyote vya Ushirika ndani wilaya ya Geita.