Rais wa zamani Jacob Zuma amezuiwa kugombea katika uchaguzi mkuu nchini Afrika Kusini utakaofanyika mwezi Mei.
Tume ya uchaguzi nchini humo (IEC), haijatoa sababu.
Hata hivyo, hukumu yake ya 2021 na kufungwa jela kwa kudharau mahakama kutaonekana kumuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Uungaji mkono wake kwa chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK) umeonekana kuwa tishio kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), ambacho kimemsimamisha kazi Bw Zuma.
Zuma mwenye umri wa miaka 81 alihudumu kama rais kutoka 2009 hadi 2018, ambapo alilazimika kujiuzulu kwa sababu ya tuhuma za ufisadi.
hama kipya cha Bw Zuma kimepewa jina la mrengo wa zamani wa kijeshi wa ANC, na anajiona kama mrithi wa kweli wa mizizi ya mapinduzi ya chama tawala.
ANC ilikuwa ilitaka shirika la uchaguzi la Afrika Kusini kufuta usajili wa MK, lakini ombi hilo lilikataliwa Jumanne.
Bw Zuma amekuwa akiongoza kampeni za chama cha MK na lilikuwa jina la kwanza kwenye orodha ya wagombeaji wao, lakini tume ya uchaguzi ilipokea pingamizi dhidi yake kuwa huenda akawa mwanachama wa Bunge la Kitaifa.
Badala ya kumpigia kura rais moja kwa moja, Waafrika Kusini huchagua wajumbe wa Bunge la Kitaifa. Mkuu wa chama chochote anachopata wengi basi anakuwa kiongozi wa nchi.
“Katika kesi ya Rais wa zamani Zuma, ndiyo, tulipokea pingamizi, ambalo limekubaliwa,” alisema mkuu wa tume ya uchaguzi Mosotho Moepya siku ya Alhamisi.