Mkuu wa wilaya ya Iringa Komred Kheri James amewapongeza Wananchi na viongozi wa Manispaa ya Iringa kwa usimamizi bora wa usafi wa mji.
Komred Kheri James ameyasema hayo mapema leo katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi lililofanyika katika kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa.
Akizungumza katika shughuli hiyo Komred Kheri James ameeleza kuwa Manispaa na viunga vyake imekuwa na mazingira safi kutokana na mpango mzuri wa usafi unaoshirikisha Wananchi kikamilifu kwa kushiriki na kwa kuchangia gharama za usafi wa maeneo yao ya huduma na makazi.
Kupitia zoezi hilo Komred Kheri James amewasihi Wananchi kuendelea kutekeleza zoezi la usafi katika maeneo yao ili kudhibiti mripuko wa maradhi, kuweka vizuri madhari ya mji na kuepuka usumbufu unaoweza kutokana na taka kuzagaa.
Pamoja na kuwahimiza wananchi kufanya usafi na kulipia gharama za usafi, Komred anewataka Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na mitaa kuongeza kasi ya usimamizi ili kuongeza uwajibikaji wa kila mdau katika kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi na salama.
Zoezi la usafi kwa Manispaa ya Iringa imehudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, viongozi, Watendaji na watumishi wa kada zote.