Wakati serikali ya awamu ya sita ikiendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi kwenye halmashauri zote hapa nchini,mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Willium Makufwe amesema katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu pekee ya Rais Samia wameweza kupokea zaidi ya Bilioni 20 inayotumika kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya afya na elimu.
Miongoni mwa miradi inayotekelezwa wilayani humo ni pamoja na ujenzi wa ofisi za halmashauri unaoghalimu kiasi cha shilingi bilioni 2 ambapo mpaka sasa ujenzi unaendelea huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha mradi huo licha ya kuwepo kwa changamoto ya mvua.
Akizungumzia mafanikio ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan katika wilaya hiyo Makufwe amesema katika mradi wa ujenzi wa ofisi za kisasa za halmashauri wamepokea takribani Bilioni mbili ambazo zitakamilisha jengo hilo kwa kuwa vifaa vyote viko eneo la mradi ambapo mpaka sasa kiasi cha bilioni moja kimekwishatumika.
“Huu mradi tuafanya chini ya mkandarasi mjenzi MUST na mnaona hata tulivyoingia vifaa vya ujenzi vipo kwa hiyo ninachowaomba wenzetu wa MUST waongeze kasi ya ujenzi ni kweli Makete tunachangamoto mvua zinanyesha lakini watumie nafasi vizuri na wafanye kazi kwa tija ili jengo liweze kukamilika na kutoa huduma inayostahili”amesema Makufwe.
Makufwe amesema miradi kama hiyo imetekelezwa katika shule ya sekondari Iwawa madarasa 12,sekondari Usililo madarasa 12,sekondari Mount Chafukwe madarasa 12 lakini pia na miradi mingine katika sekta mbalimbali.
“Katika kipindi cha miaka hii mitatu Rais ameleta hapa Makete zaidi ya bilioni ishirini na kwa uchache tu tuna vituo vya afya karibia vitano kwa hiyo ninachowaomba wanamakete hasa wazazi na walezi lazima tuiunge mkono serikali”ameongeza Makufwe
Dkt.Jonathan Kitundu ni mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya amesema katika kipindi cha miaka mitatu wameweza kupata fedha kwa ajili ya ukarabati wa hospitali hiyo pamoja na ujenzi wa jengo la huduma za dharula ambako kumewekwa vifaa vyote vinavyoghalimu zaidi ya milioni mia tatu pamoja na maboresho makubwa ya maabara ambapo pia ukarabati na ujenzi huo umepelekea kuongezeka mapato kutoka milioni sabini mpaka milioni mia mbili.
Kwenye upande wa sekta ya elimu miongoni mwa shule iliyopata maboresho makubwa ni pamoja na shule ya sekondari ya Lupalilo ambapo makamu mkuu wa shule hiyo mwalimu Kilatu amesema shule hiyo ilikuwa na changamoto kubwa kwenye miundombinu na kuwalazimu wazazi kuchangia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo kwa tabu lakini katika awamu hii yamefanyika mabadiriko makubwa ikiwemo ujenzi wa bwalo la chakula.
Respoka Mahenge na Leokadia Nyika ni miongoni mwa wanafunzi wa shule sekondari Lupalilo wilayani Makete wamemshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa miundombinu hiyo na kuahidi kwenda kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
“Tunashukuru kwa kujengewa miundombinu hii na tunaahidi kwamba kwenda kufanya vizuri na kuongeza ufaulu wetu lakini pia tunaomba kuongezewa bweni pamoja vyoo”amesema Leokadia
Nao wananchi wilayani humo akiwemo Godfrey Kusenge na Daima Klale wanasema kwa sasa halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa na maendeleo makubwa hususani kwenye maboresho ya miundombinu huku wakibainisha kuwa awali katika maeneo mengi hususani kwenye hospitali ya wilaya ambapo vitanda vilikuwa vichache lakini pia visivyokuwa na ubora ukilinganisha na sasa.