Hatimaye Bassirou Diomaye Faye ataapishwa kama rais mwenye umri mdogo zaidi wa Senegal Jumanne hii akiahidi mageuzi ya kuendeleza ushindi wake mzuri wa uchaguzi siku 10 tu baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44 hajawahi kushika wadhifa wa kuchaguliwa lakini viongozi kadhaa wa Afrika, akiwemo Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria, wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo katika mji mpya wa Diamniadio, karibu na mji mkuu wa Dakar.
Makabidhiano rasmi ya madaraka na Rais Macky Sall yatafanyika katika ikulu ya rais huko Dakar.
Faye alikuwa mmoja wa kundi la wapinzani wa kisiasa walioachiliwa huru kutoka gerezani siku 10 kabla ya kura ya urais ya Machi 24 chini ya msamaha uliotangazwa na Sall ambaye alijaribu kuchelewesha kura.
Kampeni ya Faye ilizinduliwa akiwa bado kizuizini.
Mkaguzi huyo wa zamani wa kodi atakuwa rais wa tano wa taifa hilo la Afrika Magharibi tangu lipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960 na wa kwanza kukiri waziwazi kuwa na wake wengi.
Akifanya kazi na mshauri wake maarufu Ousmane Sonko, ambaye alizuiwa kushiriki uchaguzi, Faye alitangaza vipaumbele vyao katika hotuba yake ya ushindi: maridhiano ya kitaifa, kupunguza mzozo wa gharama ya maisha na kupambana na ufisadi.