Madaktari wa hospitali za umma nchini Kenya ambao wamekuwa kwenye mgomo tangu mwezi uliopita walikutana katika miji miwili mikuu siku ya Jumanne kujadili malalamishi yao dhidi ya serikali.
Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KMPDU, ambao unawakilisha zaidi ya wanachama 7,000, waligoma Machi 15 wakidai kulipwa malimbikizo ya mishahara yao na kuajiriwa mara moja kwa madaktari waliofunzwa.
Malimbikizo hayo yalitokana na makubaliano ya mazungumzo ya pamoja ya 2017, CBA, umoja huo ulisema.
Madaktari pia wanadai utoaji wa bima ya matibabu ya kutosha kwa ajili yao na wategemezi wao.
Muungano huo pia unataka serikali kushughulikia ucheleweshaji wa mishahara mara kwa mara na kuanza kuwalipa madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za umma kama sehemu ya kozi zao za shahada ya juu.
Waziri wa afya Susan Nakhumicha amesema serikali haiwezi kumudu kuwaajiri madaktari waliofunzwa kutokana na shinikizo la kifedha kwa kitita cha umma.
Sekta ya afya ya Kenya, ambayo madaktari wanasema haina fedha za kutosha na ina wafanyakazi wachache, mara kwa mara inakabiliwa na migomo.