Mwanafunzi mmoja amefariki nawengine wawili wamejeruhiwa baada ya kupigwa risasi wakiwa darasani katika Shule ya Viertola Nchini Finland na mwanafunzi mwenzao wa darasa moja mwenye umri wa miaka 12 ambaye alifika Shuleni akiwa na bastola na kuanza kufyatulia wenzake risasi leo April 02,2024, Polisi wa Nchi hiyo wamethibitisha.
Polisi wamesema Mwanafunzi aliyefariki ana umri wa miaka 12 pia na alifariki akiwa bado Shuleni muda mfupi baada ya kupigwa risasi huku Wanafunzi wengine wawili ambao nao pia wana umri wa miaka 12 wakipelekwa Hospitali baada ya kujeruhiwa kwa risasi hizo na hali zao ni mbaya.
Tukio hilo limetokea katika Shule hiyo ya Msingi na Elimu ya Kati yenye jumla ya Wanafunzi 800 wa umri wa kuanzia miaka 7 hadi 16 ikiwa na Wafanyakazi 90 wakiwemo Walimu na ipo Jiji la Vantaa Kaskazini mwa Mji Mkuu wa Nchi hiyo uitwao Helsinki.
Mtoto huyo alijaribu kukimbia baada ya kuwaona Polisi lakini wamemkamata kwa njia laini bila kutumia nguvu wala kumuumiza na kwakuwa Wanafunzi chini ya miaka 15 hawawajibiki kwa makosa ya jinai Nchini humo, Mtoto huyo hajawekwa Mahabusu na badala yake amehifadhiwa sehemu chini ya uangalizi wa Maafisa wa Ustawi wa Jamii huku uchunguzi wa mauaji ukiendelea.
Uchunguzi wa awali unaonesha Mtoto huyo alitumia silaha ambayo imesajiliwa kwa jina la Mtu mmoja wa Famila yake….umiliki wa silaha umeenea kwa kasi Finland na Mtoto aliyefikisha miaka 15 anaruhusiwa kuwa na leseni ya kutumia silaha ya Mtu mwingine.