Miili sita ya wafanyakazi wa kigeni wa kutoa misaada waliouawa katika shambulizi la Gaza ilitarajiwa kusafirishwa kutoka katika eneo lenye vita la Palestina kupitia Misri siku ya Jumatano huku Israel ikikabiliwa na kihoro cha ghadhabu kutokana na vifo vyao.
Mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na Israel yaliwauwa wafanyakazi saba wa shirika la kutoa misaada la chakula la World Central Kitchen lenye makao yake nchini Marekani siku ya Jumatatu katika shambulio ambalo mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilitaja kuwa “lisilofaa” na “matokeo yasiyoepukika ya jinsi vita vinavyoendeshwa”.
Mabaki ya wafanyakazi sita wa kimataifa, waliouawa pamoja na mfanyakazi mwenzao wa Kipalestina, yalipangwa kutolewa Gaza kupitia kivuko cha Rafah na Misri, alisema Marwan Al-Hams, mkurugenzi wa Hospitali ya Abu Youssef Al-Najjar ya mji huo.