Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wanakutana Alhamisi kusherehekea miaka 75 ya muungano wao, baada ya kukubaliana kuanza kupanga jukumu kubwa la kuratibu msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Katika siku ya pili ya mkutano huko Brussels, mawaziri wataashiria kutiwa saini huko Washington mnamo Aprili 4, 1949, kwa Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini ambao ulianzisha muungano wa kisiasa na kijeshi wa kupita Atlantiki.
“Tunapokabiliana na ulimwengu hatari zaidi, uhusiano kati ya Ulaya na Marekani Kaskazini haujawahi kuwa muhimu zaidi,” Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema Jumatano.
NATO ilianza na wanachama 12 kutoka Amerika ya Kaskazini na Ulaya, iliyoanzishwa ili kukabiliana na hofu inayoongezeka kwamba Umoja wa Kisovyeti ulikuwa tishio la kijeshi kwa demokrasia za Ulaya.
Miaka 75 sasa , NATO ina wanachama 32 na imechukua tena nafasi kuu katika masuala ya dunia, baada ya vita vya Urusi nchini Ukraine kusababisha serikali za Ulaya kuiona Moscow kama tishio kubwa la usalama.