Rais Samia Suluhu Hassan amesema udhibiti hafifu wa mifumo ya ukusanyaji, utunzaji na utumiaji wa taarifa binafsi katika taasisi mbalimbali zilizokusanywa ulisababisha udukuzi na kuvuja kwa taarifa.
Rais Samia ameyasema hayo Aprili 3, 2024 katika uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) uliofanyika ndani ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema, siku za nyuma kuna visa vilitokea kwa kuvuja kwa taarifa binafsi za taasisi na watu binafsi upande wa taarifa zilizochukuliwa na hoteli na hospitali kuhusu wateja wao kuvuja na kuleta hathari kwa wahusika.
“Yote yalisababishwa na udhibiti hafifu wa mifumo ya ukusanyaji, utunzaji na utumiaji wa taarifa binafsi katika taasisi mbali mbali zilizokusanywa na hii ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeweka bayana kulindwa kwa taarifa binafsi za watu au kulindwa kwa haki za binadamu lakini miongoni mwa haki za binadamu ni kulindwa kwa haki za faragha, kwa mujibu wa ibara ya 16 (1) kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi ya maisha yake binafsi na familia yake.
“Ibara ya 16 (2) ya Katiba ilizitaka mamlaka za nchi kuweka utaratibu wa kisheria kulinda haki ya faragha nchini.
“Kwa upande mwingine ibara ya 12 ya tamko la kimataifa la haki za kibinadamu 1948 inayataka mataifa kuweka utaratibu unaohakikisha mtu yoyote haingiliwi faragha yake, familia yake nyumbani au kwenye makazi yake wala kuvunjiwa heshima utu na hadhi yake,” amesema.
Amesema, kwa upande wa Kikanda suala la ulinzi wa faragha limepewa kipaumbele katika jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya SADC kupitia miongozo mbali mbali, Umoja wa Afrika nao kupitia mkataba wa mwaka 20214 unasisitiza faragha.