Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio ametangaza utumiaji wa dawa za kulevya nchini humo kuwa janga la kitaifa na kuelezea hatua za kukabiliana na dawa za kulevya zinazopendwa na vijana.
Kush, mchanganyiko wa dawa yenye athari sawa na bangi na tramadol, imekuwa ikienea nchini kwa miaka mingi haswa katika maeneo ya mijini
“Nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na tishio lililopo kutokana na athari mbaya za dawa za kulevya na uraibu wa dawa za kulevya, haswa kush,”
Rais Bio alisema katika hotuba kwa taifa siku ya Alhamisi. “Kush hii mbaya inaleta athari mbaya kwa jamii zetu.”
Alisema serikali yake inajitahidi kusambaratisha mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya nchini.
Dawa hiyo ambayo pia inajulikana kama K2 inapatikana kwa urahisi kwa vijana wasio na ajira wanaotafuta kutoroka kutoka kwa umaskini na kiwewe cha maisha.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa ulaji wa kush unaweza kusababisha uharibifu wa kudumu wa ubongo na vitendo vya kujiua.
Mwezi Februari, serikali ya Sierra Leone ilianzisha kituo cha kurekebisha tabia kwa wahasiriwa wa matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kuunda kikosi kazi cha mawaziri.
Majirani wa Sierra Leone, Guinea na Liberia pia wanapigania kuzuia ongezeko la matumizi ya kush.
Nchini Liberia, Rais Joseph Boakai alitangaza matumizi ya dawa za kulevya kuwa dharura ya afya ya umma na kutangaza kamati ya kukabiliana na tishio lililopo, wakati wa hotuba yake ya kwanza ya taifa mwezi Januari.