Watetezi wa haki za mashoga nchini Uganda, sasa wanaitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo zaidi kwa utawala wa Kampala ili ibatilishe sheria kali iliyopitishwa mwaka uliopita kuhusu watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Wito wao ni baada ya mahakama ya kikatiba kutupilia kesi iliyokuwa imefunguliwa kupinga sheria hiyo.
Mwanaharakati Frank Mugisha amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa uamuzi uliochukuliwa na mahakama ulikuwa mbaya na wa kusikitisha na kwamba unapaswa kusababisha vikwazo zaidi kwa Uganda.
Mugisha amesema hakuna mfadhili anayepaswa kufadhili chuki dhidi ya LGBTQ+ na ukiukaji wa haki za binadamu kwa taifa lolote linalopinga ushoga.
Wito wao umekuja wakati huu, baraza la tume ya haki za binadamu la umoja wa Mataifa, ikipitisha azimio la kwanza linalolenga kuwalinda watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.